0





Stakabadhi ghalani siyo neno geni masikioni mwa Watanzania hasa, wanaoishi katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Singida, Kilimanjaro na Morogoro.
Wakati wakazi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani wakiutambua mfumo wa stakabadhi ghalani kwa sababu ya zao la korosho, mfumo huo unatumika katika mkoa wa Singida katika zao la alizeti, Kilimanjaro kwa zao la kahawa na mkoani Morogoro kwenye zao la mpunga.
Huu ni mfumo wa kukusanya mazao pamoja kwenye ghala maalumu lililosajiliwa na Serikali kwa lengo la kuyauza kwa bei ya ushindani.
Katika mfumo huo, asasi za fedha zinaweza kutoa mkopo kwa dhamana ya mazao hayo yaliyohifadhiwa kwenye ghala na malipo ya wakulima yanafanywa baada ya mazao hayo kuuzwa.
Nyaraka kutoka Bodi ya Korosho Tanzania zinaonyesha kuwa, zao la korosho lilikuwa la kwanza nchini kuuzwa kwa kutumia mfumo huo.
Zinasema korosho zilianza kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani katika msimu wa mwaka 2007/2008 mkoani Mtwara na baadaye mkoani Lindi katika msimu wa mwaka 2008/ 2009.
Mikoa ya Ruvuma na Pwani ilianza kutumia mfumo huo wa stakabadhi ghalani katika msimu wa 2009/2010 na Mkoa wa Tanga ukaingia kwenye utekelezaji wake katika msimu wa 2011/2012.
Faida ya stakabadhi ghalani?
Kabla ya mfumo huo kuanza kutumika wafanyabiashara walikuwa wananunua korosho moja kwa moja kutoka kwa wakulima kupitia bei dira.
Katika utaratibu huo, wakulima walikuwa wakipunjwa malipo kutokana na ukweli kwamba wafanyabiashara walikuwa wakitumia vipimo vyao ambavyo vilifanya wakulima hao walipwe bei sawa au pungufu ya bei dira.
Bei dira ni nini?


Bei dira ni bei ya kujipanga kibiashara tu. Bei halisi hupatikana sokoni. Bei dira siyo mkataba kati ya chama cha msingi na wakulima. Wakulima hugawiwa fedha zao baada ya kulipwa kwa gharama za mauzo.



Post a Comment

 
Top